
Niliwahi sali Misa na kusikia hili jambo pale Parokia ya Mwenyeheri Anuarite Makoka – Tabata jijini Dar es salaam.
IKO HIVI: Mchakato huu ulianza rasmi tarehe 13 Mei 2005 baada ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuridhia ombi la Jimbo Katoliki la Musoma.
Baada ya hapo, Papa Benedicto XVI alitangaza rasmi Nyerere kuwa “Mtumishi wa Mungu” (Servant of God).
Na hii ni hatua ya kwanza kabisa katika safari ya utakatifu.
HATA HIVYO: Mchakato huu ni mrefu sana.
Unachukua miaka mingi na haumaanishi kuwa tayari ameshatangazwa kuwa mtakatifu bali bado yupo kwenye hatua ya Mtumishi wa Mungu.
UTARATIBU MZIMA: Hivi ndivyo utaratibu wa Kanisa Katoliki Unavyofanya Kazi kumtangaza mtu kua Mtakatifu: Muumini, mlei au kiongozi wa Kanisa kutangazwa kuwa Mtakatifu, ni lazima apitie hatua zifuatazo:
1. Mtumishi wa Mungu: Hii ndiyo hatua ambayo Mwalimu Nyerere yupo kwa sasa. Inaanza baada ya maombi ya kijimbo kukubaliwa na Vatican.
Katika hatua hii, Kanisa linaunda mahakama maalumu kuchunguza maisha yake, maandiko yake, na ushuhuda wa watu walioishi naye ili kuthibitisha kama aliishi maisha ya kishujaa ya kiimani na kimaadili.
2. Mtukuka: Hatua hii inafikiwa baada ya Vatican kupitia ripoti ya uchunguzi wa kijimbo na kujiridhisha kuwa mtu huyo alikuwa na fadhila za kishujaa (heroic virtues)
3. Mwenyeheri: Hapa ili mtu atangazwe kuwa Mwenyeheri, ni lazima kuwepo na muujiza mmoja uliothibitishwa kisayansi na kitiba uliotokea kwa njia ya maombezi yake.
Mfano; mtu kupona ugonjwa sugu usiotibika baada ya kumwomba Mungu kupitia Nyerere
4. Mtakatifu: Baada ya kuwa Mwenyeheri, unahitajika muujiza wa pili uliothibitishwa ili awekwe rasmi kwenye orodha ya watakatifu wa Kanisa ulimwenguni.
UHALISIA: Mchakato huu unaendelea katika ngazi ya uchunguzi wa kijimbo na ukusanyaji wa ushuhuda.
Hata hivyo Kanisa linatambua kuwa Nyerere alikuwa Mkristo mcha Mungu, aliyehudhuria Misa Takatifu kila siku popote alipokuwa, alifunga na kusali, na aliongoza Tanzania kwa;
Uadilifu. Unyenyekevu, na Upendo kwa maskini bila kujali vyeo vyake vya kisiasa.
Tuzidishe maombi kufanikisha mchakato huu. Asante…!
Karibumedia.rw
